Rais Uhuru Kenyatta amehimiza ulimwengu kuwapatia vijana nafasi za uongozi.

Rais Uhuru Kenyatta amehimiza jamii ya kimataifa kuanza kuona na kushirikisha vijana kama mali yenye thamani kwa wakati huu na  wala sio ahadi ya siku zijazo.

Rais alisema iwapo watatunzwa vyema na kupewa nafasi zinazofaa, vijana wana uwezo usio na kikomo wa kuleta mabadiliko makubwa.

Alisema uamuzi wake kuwateuwa vijana katika nafasi za juu serikalini ni hatua inayokusudiwa kuwapa vijana nafasi kuwanasihi na kuwatayarisha kwa nyadhifa kuu zaidi serikalini.

Rais aliuambia mkutano huo, ambao pia ulihudhuriwa na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ubunifu na Vijana Joe Mucheru, kwamba taasisi za kijamii,  mazingira hasa mfumo wa elimu na ukosefu wa kujiamini wenyewe ni baadhi ya vikwazo ambavyo vinawazuia vijana kuafikia uwezo wao wa kuleta mabadiliko.

Rais Kenyatta alizungumzia kuhusu wajibu wa vijana wa kuleta mabadiliko katika kongamano ambalo pia lilihutubiwa na viongozi kadhaa wa ulimwengu wakiwemo Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais wa Benki ya  Dunia David Malpass na Mkurugenzi wa Shirika la Fedha Ulimwenguni Kristalina Georgieva.

Kiongozi wa Taifa alisema hayo Jumanne jioni katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana unaotambulika kama United Nations Generation Unlimited.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress alihimiza mataifa kutumia mawasiliano ya kidijitali kubuni nafasi kwa vijana.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown alihimiza makundi ya G7 na G20 kutenga dola bilioni 10 za Kimarekani kwa upanuzi wa teknolojia ya kidijitali  ilhali Bw David Malpass alisema Benki ya Dunia inashirikiana na washikadau kutatua tofati za mahitaji ya kidijitali miongoni mwa mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *