Mawaziri Wawili Wafariki Kutokana Na Korona Malawi

Mawaziri wawili nchini Malawi wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Waziri wa uchukuzi, Sidik Mia na mwenzake wa serikali za wilaya, Lingston Belekanyama waliaga dunia katika hospitali tofauti hapo jana.

Hayo ni kwa mujibu wa waziri wa habari nchini Malawi, Gospel Kazako.

Mwishoni mwa wiki rais Lazarus Chakwera alitoa hotuba maalum kwa taifa kupitia redio akihimiza uzingatiaji wa masharti ya kuzuia msambao wa Covid-19 kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi na vifo.

Wakati uo huo waziri wa afya wa Taiwan, Chen Shih-chung leo ameripoti kisa cha kwanza cha maambukizi ya aina mpya ya virusi vya Korona katika kisiwa hicho.

Mgonjwa huyo alikuwa amezuru jamhuri ya Eswatini ambayo zamani ilijulikana kama Swaziland. Waziri huyo amesema kuanzia alhamisi mtu yeyote aliyezuru Eswatini katika muda wa siku 14 zilizopita lazima aende karantini na kupimwa katika hospitali ya serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *