Aprot na Chespol kuongoza mbio za nyika za Magereza Jumamosi

Bingwa wa zamani wa mbio za nyika barani Afrika Alice Aprot ni miongoni mwa majina tajika yatakayojitokeza kutimka mbio za nyika za idara ya magereza Jumamosi katika uwanja wa chuo cha makurutu KPTC  mjini Ruiru.

Aprot atarejea kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miezi 6 akiwa katika likizo  baada ya kujifungua.

Mwanariadha huyo ambaye pia ni bingwa wa Afrika katika mbio za mita 10000 mwaka 2016 mjini Durban Afrika Kusini atatumia mashindano hayo kurejea katima hali shwari kwa majaribio ya kitaifa ya mbio za nyika mwezi ujao katika kaunti ya Kisii kuwania tiketi ya kwenda Lome Togo mwezi Machi kwa mashindano ya bara Afrika.

Wanariadha wengine tajika watakaokata mbuga Jumamosi ni pamoja na bingwa wa dunia katika mita 3000 kuruka viunzi na kidimbwi  cha maji kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2018 Celphine Chespol,bingwa wa All Africa Games  katika mita  5000 mwaka 2019 Lillian Kasait,mshindi wa nishani ya fedha ya mita 5000 katika michezo ya All Africa  mwaka 2015 Rosemary Wanjiru na Sandrafelis Chebet.

Mbio za wanaume zitamshirikisha bingwa wa dunia wa mita 1500 Timothy Cheruiyot atakayetimka kilomita 10 kujiweka katika hali shwari.

Washiriki wengine kwa wanaume ni Charles Mneria aliyetwaa ubingwa katika mbio za msururu wa Mosoriot mwezi uliopita ,bingwa mtetezi wa mbio hizo Peter Emase,mshindi wa shaba ya Olimpiki mwaka 2012 katika mita 5000 Thomas Longosiwa,Mangata Ndiwa ,Wilfred Kimitei aliyenyakua fedha ya Afrika katika mita 10000 na bingwa wa Jumuiya ya madola katika mita 1500 mwaka 2010 Silas Kiplagat.

Wanariadha bora wataiwakilisha magereza katika mashindano ya kitaifa mwezi ujao mjini Kisii kuwania tiketi ya kushiriki mashindano ya Afrika mjini Lome Togo mwezi Machi mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *