Serikali Ya Kaunti Ya Mombasa Yasema Haitasitisha Shughuli Zake

Shughuli za kawaida katika Kaunti ya Mombasa zitaendelea licha ya baraza la magavana kutangaza kusitishwa kwa shughuli zote za Kaunti kuanzia leo.

Katibu wa Kaunti ya Mombasa  Dennis Lewa amesema kwamba Kaunti hiyo haiwezi kuchukua mwelekeo huo hadi itakapopata ruhusa kutoka kwa Baraza la Mawaziri  la Kaunti hiyo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Lewa amesema wanatarajia kukutana na baraza hilo ili kujua mwelekeo utakaochukuliwa.

Lewa amekiri kwamba Kaunti ya Mombasa ni miongoni kaunti ambazo zimeathiriwa na kucheleweshwa kwa fedha za kaunti kufuatia mvutano unaoendelea katika bunge la seneti.

Amesema imekuwa vigumu kwa utekelezwaji wa miradi mpya iliyokuwa imeidhinishwa huku baadhi ya miradi iliyokuwa inaendelea kutekelezwa ikikwama.

Ameeleza wasiwasi kwa wafanyakazi wa Kaunti hiyo kulipwa mishahara yao ya mwezi huu kufuatia uhaba wa fedha unaoikumba Kaunti hiyo.

Jana Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya aliwataka magavana kutoa ilani ya kuwatua wafanyakazi katika likizo ya lazima kwa muda wa wiki mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *