Mwanaolimpki Jipcho aaga dunia

Mwanariadha mstaafu Ben Jipcho aliyeshinda nishani ya fedha katika michezo ya Olimiki mwaka 1972 nyuma ya mwenzake Kipchoge Keino ameaga dunia.

Kulingana na mwanawe Ruth Jipcho, mwanariadha huyo mkongwe ambaye alikuwa na umri wa miaka 77 aliaga dunia leo alfajiri katika hospitali ya Eldoret ambako amekuwa akipata matibabu.

Daktari ambaye amekuwa akimhudumia alisema kuwa hali yake ilidhoofika baada ya viungo mbali mbali mwilini mwake kukosa kufanya kazi inavyostahili. Jipcho alishinda nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5000 kwenye michezo ya bara Afrika mwaka 1973.

Kisha akashinda nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5000 na elfu tatu kuruka vihunzi na kidimbwi cha maji katika michezo ya Jumuiya ya madola iliyoandaliwa jijini Christchurch, New Zealand.

Waziri wa michezo Amina Mohammed kwenye risala ya rambi rambi iliyochapishwa kwenye mtandao wa twita alisema kuwa alipokea habari za kifo cha mwanariadha huyo mkongwe kwa huzuni kubwa na kwamba atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa wanariadha bora humu nchini ambao ufanisi wao uliinua jina la Kenya katika ngazi za kimataifa, kuanzia mwaka 1968 wakati wa michezo ya Olimpiki jijini Mexico.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *