Manangoi asikitishwa na habari za kupigwa marufuku

Aliyekuwa bingwa wa dunia katika mbio za mita 1500 mwaka 2017 Elijah Manangoi, amesema kuwa amesikitishwa na habari za kupigwa marufuku na kitengo cha uadilifu riadhani baada ya kuwepa uchunguzi wa dawa za kusisimua misuli mara tatu.

Manangoi aliyenyakua nishani ya fedha katika mashindano ya riadha ya dunia mwaka 2015 jijini Beijing na kisha akanyakua nishani ya dhahabu jijini London miaka miwili baadaye amesema marufuku hiyo haihusiani na utumizi wa dawa za kusisimua misuli.

Manangoi alikuwa mmoja wa wanariadha wanne wa humu nchini ambao walipigwa marufuku kwa muda na kitengo cha Uadilifu wa Riadha huku wakisubiri kusikizwa kwa kesi zao kikamilifu.

Wanariadha wengine wa humu nchini ambao wamesimamishwa riadhani ni pamoja na Patrick Siele ambaye amesimamishwa kwa muda baada ya kudaiwa alikwepa, kukataa au kukosa kuwasilisha sampuli kwa wachunguzi.

Mercy Kibarus alipigwa marufuku kwa muda wa miaka minane baada ya kupatikana na hatia ya utumizi wa dawa za kusisimua misuli, kwa mara ya pili katika muda wa miaka 10.

Kenneth Kipkemoi pia alisimamishwa riadhani kwa muda wa miaka miwili baada ya kubainika kuwa ni mtumizi wa dawa zilizoharamishwa aina ya ‘terbutaline’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *