Kamati ya seneti kuhusu Corona yaibua maswali dhidi ya makabiliano ya corona Kilifi

Kamati ya seneti ya masuala ya corona imezuru kaunti ya Kilifi ili kutathimini jinsi serikali ya kaunti hiyo ilivyojipanga katika kukabiliana na janga la Corona.

Kamati hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake Silvia Mweni Kasanga imesema ziara hiyo imedhihirisha kuwa ripoti ya matumizi ya shilingi million 205 kutoka kwa serikali kuu ambayo imetolewa na idara ya afya kaunti hiyo hailingani na ripoti ya msimamizi wa bajeti nchini.

Kasanga ameeleza kuwa kwa sasa kamati hiyo inasubiri ripoti ya mwisho kutoka kwa msimamizi wa bajeti ili kubainisha matumizi halisi ya fedha hizo.

Kulingana na seneta wa Mombasa Muhameed Faki, ziara hiyo pia imedhihirisha kuwa kaunti hiyo haijajitayarisha vilivyo katika kukabiliana na masuala ya corona.

Faki ameeleza kuwa ukosefu wa vifaa Madhubuti vya wagonjwa mahututi umepelekea wagojwa wa corona kutumwa katika kaunti jirani ya Mombasa kwa matibabu.

Ziara hiyo itaendelezwa hadi kaunti ya Kwale baada ya kamati hiyo kuzuru kaunti ya Mombasa hapo jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *