Bunge la Taifa kurejelea vikao vyake leo alasiri

Kuongezeka visa vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 humu nchini kunaonekana kuongeza shinikizo kwa utekelezaji kazi ya bunge, ambapo bunge la taifa kwa mara nyingine linataka kubadili kalenda yake ili kupunguza utangamano wa wabunge.

Bunge la taifa ambalo linarejelea vikao vyake leo alasiri baada ya likizo ya wiki tatu sasa linataka liwe na kikao kimoja pekee kwa wiki.

Hoja ya kubadili kalenda yake inatarajiwa kuwasilishwa na kiongozi wa walio wengi Dkt. Amos Kimunya leo alasiri, huku bunge la taifa likipendekeza liwe na vikao siku ya Jumatano pekee kuanzia tarehe 5 mwezi ujao.

Kikao hicho kulingana na hoja hiyo kitaanza saa nne asubuhi kwa kikao cha asubuhi na saa nane na nusu kwa kikao cha alasiri.

Kwenye hatua ya awali ya kubadili kalenda yake, bunge la taifa lilikuwa na vikao siku za Jumanne na Alhamisi pekee.

Janga la korona pia halijasaza vikao vya kamati za bunge ambavyo kwa sasa vinaendeshwa kwa njia ya mtandao.

Hivi majuzi mkuu wa utumishi wa umma Joseph kinyua aliandikia bunge barua kulifahamisha haja iliyopo ya kuzingatia mikutano inayofanywa kwa njia ya mtandao wabunge wanapotangamana na maafisa wa serikali ili kudhibiti msambao wa ugonjwa wa COVID-19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *